https://journals.chaka-ma.com/index.php/chakama/issue/feedchama Cha Kiswahili Afrika Mashariki2023-03-26T12:58:51+00:00DR. JAMES ONTIERImharirimkuuchakama@gmail.comOpen Journal Systems
CHAMA CHA KISWAHILI AFRIKA MASHARIKI (CHAKAMA)

Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA) ni chama cha wahadhiri wa Kiswahili wa vyuo vikuu katika ukanda wa Afrika Mashariki. Chama hiki kilizinduliwa tarehe 7 Julai mwaka 2002 na wajumbe wa warsha ya wataalamu wa Kiswahili wa vyuo vikuu vya Afrika Mashariki wakati wa mkutano uliofanyika katika Hoteli ya Eland, Arusha, Tanzania.
https://journals.chaka-ma.com/index.php/chakama/article/view/1KISWAHILI NA LUGHA NYINGINE ZA KIAFRIKA KATIKA MAENDELEO YA AFRIKA MASHARIKI2023-03-26T11:36:34+00:00Nathan Ogechiogechi@chaka-ma.com
Makala hii inajaribu kutathmini namna ambavyo matumizi ya Kiswahili na lugha nyingine za KiAfrika yanaweza kuchangia maendeleo chanya na hasi. Dhana ya maendeleo imefafanuliwa ili kujumuisha sio tu ukuaji kiuchumi bali pia ukuaji wa demokrasia inayoruhusu ushiriki wa wananchi wote katika maamuzi juu ya masuala ya jamii wanamoishi. Mjadala umejikita katika maeneo matatu makuu ya maendeleo: uongozi na siasa; elimu na sekta ya uchumi isiyo rasmi. Kwa kutoa mifano ya matukio katika jamii pamoja na ithibati ya miradi ya utafiti iliyowahi kuendeshwa, imedhihirishwa kwamba Kiswahili na lugha nyingine za KiAfrika ni nguzo murua ambazo haziwezi kupuuzwa katika maendeleo ya Afrika Mashariki. Imeonyeshwa kwamba ijapokuwa kuna maendeleo hasi pamoja na changamoto wakati lugha hizi zinapotumika, upungufu uliobainishwa hautoshi kuzitupilia mbali lugha hizi. Hii ni kwa sababu kuna suluhu kwa changamoto hizo na kadri lugha yoyote inavyozidi kutumika ndivyo inazidi kuimarika ili kutekeleza majukumu ya maendeleo ya jamii.
2022-04-12T00:00:00+00:00Copyright (c) 2022 chama Cha Kiswahili Afrika Masharikihttps://journals.chaka-ma.com/index.php/chakama/article/view/2RIWAYA YA KISWAHILI KAMA KIOO CHA UTAMADUNI WA AFRIKA MASHARIKI: MAENDELEO YANAHUSIKAJE?2023-03-26T12:07:47+00:00Mwenda Mbatiahmwenda@chaka-ma.com
Makala haya yanaegemea mtazamo wa kinadharia wa kwamba fasihi huakisi maisha halisi ukiwemo utamaduni. Hivyo basi, riwaya ya Kiswahili ambayo ni zao la wasanii wa Afrika Mashariki, inaweza kuchukuliwa kama kioo cha utamaduni wa kanda hii. Makala haya yanachunguza vipengele vya utamaduni huo ambavyo riwaya teule zinashughulikia, na kujadili ikiwa kwa kufanya hivyo riwaya hizo zinachangia katika maendeleo ya jamii zinazohusika. Hivi ni kwa kuchukulia (kufuatana na nadharia tunayoitumia) kwamba watunzi wa riwaya huwa wamejitolea kuchangia maendeleo ya jamii zao. Kwa hali hii riwaya walizotunga zinaweza kuchukuliwa kama fasihi pendelevu. Data ambayo tutatumia katika uchunguzi huu ni riwaya kumi ambazo zimeteuliwa kimakusudi kuwakilisha awamu muhimu za ukuaji wa utanzu unaohusika na pia maeneo wanakotoka waandishi wake.
2022-04-12T00:00:00+00:00Copyright (c) 2022 Chama Cha Kiswahili Afrika Masharikihttps://journals.chaka-ma.com/index.php/chakama/article/view/3ISIMU YA KIJANI YA MAJINA YA MIEZI KATIKA RUKIGA2023-03-26T12:13:56+00:00Leonard Chacha Mwitamwita@chaka-ma.comAidah Mutenyomutenyo@chaka-ma.comMartin Muleimulei@chaka-ma.com
Lugha haipatikani katika ombwe. Lugha ni matokeo ya mtagusano baina ya watu wanaoizungumza na mazingira yao. Kwa kweli, kuna uhusiano mkubwa baina ya mazingira, lugha na wazungumzaji wake. Makala hii itajikita katika majina ya kiasili na majina ya kisasa ya miezi ya mwaka katika Rukiga. Rukiga ni lugha ya Kibantu inayozungumzwa Kusini Magharibi mwa nchi ya Uganda, hasa eneo la Kabale. Majina asili ya miezi ya Rukiga yametokana na mahusiano ya watu na mazingira yao na yanaonyesha namna lugha inavyoweza kutumiwa kuzungumzia mazingira na kumwezesha binadamu kuyatawala. Majina haya ya kiasili yanaeleza mengi kuhusu mazingira na hali ya miezi husika. Katika utafiti huu, juhudi zilifanywa kubaini ikiwa matumizi ya majina ya ‘kisasa’ yanaakisi mabadiliko katika jamii kuhusu mtazamo wao juu ya mazingira. Uchunguzi huu uliongozwa na nadharia ya Filosofia ya Ikolojia (Ecosophy). Uchanganuzi uliofanywa unaonyesha kwamba majina ya ‘kisasa’ ya miezi yanadhihirisha ukosefu wa mtagusano kati ya wazungumzaji na mazingira kama ilivyokuwa katika majina ya kiasili. Makala inapendekeza mbinu mbalimbali za kuwezesha kizazi cha sasa kuyafahamu na kuyatumia majina ya asili ya miezi ya mwaka.
2022-04-12T00:00:00+00:00Copyright (c) 2022 Chama Cha Kiswahili Afrika Masharikihttps://journals.chaka-ma.com/index.php/chakama/article/view/4KISWAHILI NA MAENDELEO YA JUMUIA YA AFRIKA MASHARIKI2023-03-26T12:20:28+00:00Ayub Mukhwanaayub@chaka-ma.com
Dhana za maendeleo, hasa kupitia kwa chombo kama lugha, ni tata na telezi. Makala hii imejitokeza na fasiri zake za maendeleo kama dhana na ndizo ambazo kwamo yaliyomo katika makala hii yamejikita. Vyombo mbalimbali vya kiuchumi na kijamii barani Afrika, na hasa Afrika Mashariki, vimerejelewa huku mchango na mafungamano yake na lugha ya Kiswahili katika maendeleo ya Jumuia ya Afrika Mashariki vikijadiliwa. Yaliyomo katika makala hii ni ya kinadharia na vilevile kimatendo ambapo yote yanalenga katika kutoa nafasi ya lugha ya Kiswahili katika maendeleo ya Jumuia ya Afrika Mashariki. Hitimisho la makala hii ni kuwa, pamoja na changamoto zinazojitokeza, Kiswahili kinao mchango mkubwa katika maendeleo ya kielimu, kiuchumi, kisayansi na kiteknolojia, pamoja na ya kisiasa katika Jumuia ya Afrika Mashariki.
2022-04-12T00:00:00+00:00Copyright (c) 2022 Chama Cha Kiswahili Afrika Masharikihttps://journals.chaka-ma.com/index.php/chakama/article/view/5FAHARASA KATIKA DIWANI ZA SAID AHMED MOHAMED: VIJENZI NA TIJA ZAKE2023-03-26T12:24:29+00:00Hassan R. Hassan Hassanhassan@chaka-ma.com
Makala hii inajadili faharasa katika diwani za Said Ahmed Mohamed kwa kuangazia vijenzi na tija zake. Faharasa ni sehemu muhimu katika vitabu vya fani mbalimbali. Sehemu hii aghalabu hujumuisha maneno magumu yaliyotumiwa ndani ya kitabu husika. Kupitia faharasa, wasomaji wamekuwa wakifaidika kwa kupata ufafanuzi wa maneno yaliyotumika kitabuni. Makala hii imetokana na uchunguzi wa kimaktaba. Mjadala unafanywa kwa kuegemezwa katika diwani tatu za Said Ahmed Mohamed ambazo ni ‘Sikate Tamaa’ (1980), ‘Kina cha Maisha’ (1984) na ‘Jicho la Ndani’ (2002). Matokeo ya uchunguzi yameonesha kuwa faharasa katika diwani teule zinaundwa na: maneno ya kilahaja, maneno ya kale na maneno ya kishairi. Aidha, kuna maneno yaliyogeuzwa kuwa na sura ya kizamani, vikasiri na mazidadi. Pia, uchunguzi umezibaini tija ziletwazo na faharasa hizo kuwa ni kupevusha taaluma ya leksikografia, kuhifadhi msamiati wa lugha, kufundisha lugha na kuonesha namna bora ya kufanya ukiushi katika ushairi. Aidha, faharasa huonesha ukwasi na umbuji wa lugha wa mtunzi na hujenga uhusiano wa mtunzi na jamii yake.
2022-04-12T00:00:00+00:00Copyright (c) 2022 Chama Cha Kiswahili Afrika Masharikihttps://journals.chaka-ma.com/index.php/chakama/article/view/6MCHANGO WA RUNUNU KATIKA MAENDELEO YA KISWAHILI2023-03-26T12:28:14+00:00Basilio Gichobi Munganiamungania@chaka-ma.com
Kiswahili ni lugha inayokua na kusambaa katika maeneo mbalimbali ulimwenguni tena kwa kasi sana. Siku za hivi karibuni, nchi nyingi barani Afrika (zikiwemo Afrika Kusini, Rwanda, na Zimbabwe) zimeamua Kiswahili kifundishwe katika shule za nchi hizo, na zingine zimekubali Kiswahili kiwe mojawapo ya lugha rasmi za nchi (Rwanda). Kwa upande mwingine, matumizi ya rununu yameenea kwa mapana na marefu, hususan kutokana na upenyaji, kukubalika, na matumizi yake. Asilimia kubwa ya raia wa nchi ambapo Kiswahili kinatumika ama wanamiliki simu tamba au/na wana uwezo wa kutumia simu tamba katika maisha yao ya kila siku (kama vile matumizi ya huduma ya M-Pesa). Makala hii inahoji kuwa upatikanaji na matumizi ya rununu kwa wingi huchangia maendeleo ya jamii husika pamoja na yale ya Kiswahili. Itaangalia kwa kifupi historia ya simu tamba nchini Kenya, pamoja na kuchunguza namna raia wa nchi husika wanavyoingiliana na kuhusiana na rununu na, ikiwa wanatumia Kiswahili katika rununu katika shughuli zao za kila siku. Kadhalika, itachunguza mchango wa simu tamba katika kukuza na kuendeleza Kiswahili.
2022-04-12T00:00:00+00:00Copyright (c) 2022 Chama Cha Kiswahili Afrika Masharikihttps://journals.chaka-ma.com/index.php/chakama/article/view/7TATHMINI YA SERA ZA LUGHA KATIKA SEKTA YA ELIMU NCHINI KENYA: HALI YA SASA YA KISWAHILI KATIKA MTAALA MPYA2023-03-26T12:31:01+00:00Juliet Akinyi Jagerojuliet@chaka-ma.com
Sera ya lugha katika sekta ya elimu katika nchi yoyote ile ni muhimu kwa vile ndiyo huamua jukumu la kila lugha katika elimu. Nchini Kenya sera hizi zimepitia mabadiliko mengi yanayoweza kuangaliwa miaka ya nyuma yanayoanza wakati wa ukoloni hadi sasa. Sera hizo zinahusisha Kiingereza, Kiswahili na lugha zingine asilia. Sera hizi zimeeleza namna kila lugha inafaa kutumika katika kufanikisha shughuli za kufundisha na kujifunza katika kila kiwango. Ingawa lugha ya Kiswahili inatambulika kama lugha rasmi na ya taifa nchini Kenya, katika mtaala mpya wa elimu haijapewa nafasi muhimu inavyostahili. Hali hii huenda imetokana na sera za lugha za awali kuanzia wakati wa ukoloni hadi sasa. Makala hii inatathmini sera za lugha katika sekta ya elimu nchini Kenya kuanzia wakati wa ukoloni hadi sasa ili kuonesha namna sera hizo zimachangia hali ya sasa ya Kiswahili katika mtaala mpya. Kadhalika, makala hii inaangazia nafasi ya Kiswahili katika mtaala mpya huku ikitoa mapendekezo.
2022-04-12T00:00:00+00:00Copyright (c) 2022 Chama Cha Kiswahili Afrika Masharikihttps://journals.chaka-ma.com/index.php/chakama/article/view/8KISWAHILI KAMA NYENZO YA KUFUNDISHIA ELIMU YA URAIA KATIKA TAASISI ZA ELIMU NCHINI KENYA2023-03-26T12:33:10+00:00Alex Umbima Kevogokevogo@chaka-ma.comMosol Kandagor KandagorKandagor@chaka-ma.com
Lugha ya Kiswahili imepata hadhi kikatiba na kuwa lugha ya taifa na lugha rasmi nchini Kenya. Isitoshe, Kiswahili ndiyo lugha inayotumiwa na Wakenya wengi kwa ajili ya mawasiliano yao kila siku. Katiba ya Kenya inatambua umuhimu wa lugha ya Kiswahili kama chombo cha kukuzia umoja, wiano na utangamano wa kitaifa. Dhima ya Kiswahili kama lugha inayowaungunisha Wakenya wanaotoka katika maeneo na matabaka mbalimbali kitaifa haiwezi kusisitizwa bali inaeleweka wazi. Kutokana na uelewa huu, tunahoji kuwa lugha ya Kiswahili pamoja na hadhi yake kikatiba, inaweza kutumiwa kama wenzo wa kufundishia na kujifinzia elimu uraia vyuoni na shuleni. Elimu uraia ni msingi wa kujenga mihimili ya uzalendo na utaifa miongoni mwa wanafunzi wanaoibuka kutoka sehemu mbalimbali za taifa. Tunahoji pia kuwa Kiswahili ni chombo thabiti kinachoweza kutekeleza jukumu hili kwa ajili ya uwezo wake wa kuwaleta pamoja Wakenya. Msimamo wetu ni kuwa haiwezekani kufundisha masuala ya utaifa na uraia kwa lugha nyingine ambayo si ya taifa. Baadhi ya masuala muhimu yanayoweza kufundishwa kupitia kwa Kiswahili ni yale yanayohusu wiano wa kitaifa, uzalendo, katiba, serikali, utawala, ugatuzi wa mamlaka, demokrasia, haki za kibinadamu, uhifadhi na utunzaji wa mazingira, umoja na utangamano, usuluhishaji migogoro kwa njia ya amani na taathira za ufisadi. Makala hii basi inalenga kuonyesha umuhimu wa kutumia Kiswahili kutekeleza kazi hii na changamoto zinazoweza kuibuka kutokana na hali hiyo.
2022-04-12T00:00:00+00:00Copyright (c) 2022 Chama Cha Kiswahili Afrika Masharikihttps://journals.chaka-ma.com/index.php/chakama/article/view/9UTAFITI WA ISIMU YA KISWAHILI KATIKA VYUO VIKUU2023-03-26T12:36:15+00:00Hanah Chaga MwaliwaMwaliwa@chaka-ma.com
Utafiti wa isimu ya Kiswahili ni nguzo muhimu ya ufundishaji na maendeleo ya Kiswahili. Ili lugha ipate kukua na kuendelea, kuna haja ya kufanya utafiti zaidi katika sarufi ya lugha husika. Kwa muda mrefu, isimu ya Kiswahili imefanyiwa utafiti na kufunzwa katika vyuo vikuu. Hata hivyo, utafiti wa isimu ya Kiswahili katika vyuo vikuu umezongwa na changamoto/matatizo si haba. Changamoto hizi zinahusu idadi ya tafiti, nadharia za isimu na umakinifu unaoendana na utafiti wa isimu ya Kiswahili vyuoni. Hali hii imechangia ufundishaji wa isimu ya Kiswahili kukumbwa na uhaba wa walimu na vitabu/marejeleo, kutofundishwa kwa nadharia za isimu na tafiti chache katika mawanda yote ya isimu ya Kiswahili. Kutokana na changamoto hizi, idadi ya wanafunzi wa isimu ya Kiswahili ni ndogo mno. Makala haya yanalenga kutathmini na kujadili changamoto zilizoko katika utafiti wa isimu ya Kiswahili vyuoni. Hususan, silabi za Kiswahili zimepewa nafasi ndogo katika utafiti na ufundishaji vyuoni. Hii ndio sababu kumekuwa na mielekeo tofautitofauti kuhusu silabi za Kiswahili. Utafiti umeonyesha kwamba silabi ina jukumu muhimu katika sarufi ya lugha yoyote ile, ikiwemo Kiswahili. Makala haya vilevile yananuia kuonyesha umuhimu wa kutafiti na kufunza silabi za Kiswahili kwa kutumia nadharia mahsusi za kiisimu. Mbali na kutathmini changamoto hizi, makala haya yanalenga kutoa mapendekezo ya kuimarisha utafiti na ufunzaji wa isimu ya Kiswahili vyuoni.
2022-04-12T00:00:00+00:00Copyright (c) 2022 Chama Cha Kiswahili Afrika Masharikihttps://journals.chaka-ma.com/index.php/chakama/article/view/10UMUHIMU WA MABADILIKO KATIKA VIWANGO MBALIMBALI VYA LUGHA YA KISWAHILI KATIKA MUKTADHA WA ISIMUHISTORIA2023-03-26T12:38:18+00:00Zainab Ali IddiIddi@chaka-ma.com
Makala hii inazungumzia umuhimu wa kutathmini mabadiliko ya lugha katika viwango mbalimbali vya lugha. Data za makala hii zimekusanywa uwandani na maktabani. Katika uchambuzi wake makala imetumia nadharia ya Isimuhistoria. Matokeo yanaonesha kwamba kufanya uchunguzi wa kihistoria katika lugha yoyote ni muhimu kwani bila kuangaliwa mabadiliko hayo, lugha haitakuwa na maendeleo. Hivyo, lugha inahitaji kuchunguzwa katika viwango vyote ili kubaini mabadiliko yaliyoingia kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni. Makala imebaini kwamba lugha ya Kiswahili imepitia mabadiliko mbalimbali katika viwango vyote vya lugha. Baadhi ya mabadiliko hayo ni potevu.
2022-04-12T00:00:00+00:00Copyright (c) 2022 Chama Cha Kiswahili Afrika Masharikihttps://journals.chaka-ma.com/index.php/chakama/article/view/11MUUNDO WA VIVUMISHI VYA LUGHA ZA MNYAMBULIKO: MFANO WA KIVUMISHI CHA KIIMENTI2023-03-26T12:40:39+00:00Kenneth Kinyua Thuranirakinyua@chaka-ma.comJames OntieriOntieri@chaka-ma.comNancy AyodiAyodi@chaka-ma.com
Kivumishi ni aina mojawapo ya maneno ambayo hutumika katika lugha sambamba na nomino ili kufanikisha mawasiliano. Ingawa tafiti nyingi zimefanywa kuhusu vivumishi, hatukuona utafiti wowote uliolenga miundo ya vivumishi katika Kiimenti. Makala haya yananuia kubainisha muundo wa kivumishi cha lahaja ya Kiimenti. Kiimenti ni mojawapo ya lahaja za Kimeru. Kimeru ni mojawapo ya lugha za Kibantu ambazo huzungumzwa nchini Kenya. Nia ya makala haya ni kuchunguza muundo wa kivumishi cha Kiimenti kwa kuongozwa na Nadharia ya Sarufi Geuza Maumbo Zalishi ambayo iliasisiwa na mwanaisimu Noam Chomsky (1957, 1965). Kupitia kwa nadharia hii, muundo wa nje na wa ndani wa kivumishi cha Kiimenti umewekwa wazi. Data ya utafiti huu ilipatikana kutokana na utafiti wa maktabani na nyanjani. Maktabani watafiti walisoma kazi mbalimbali zilizoangazia vivumishi vya Kiimenti. Utafiti wa nyanjani ulifanyika katika tarafa ya Abothuguchi Magharibi kwenye Kaunti ya Meru ambapo watafiti waliteua kimaksudi miktadha ya mikutano ya masoko na makanisa ili kukusanya data. Makala haya yanathibitisha kuwa kivumishi cha Kiimenti kinawasilisha muundo mahsusi na kikichanganuliwa kimofemiki kinaweza kuainisha mofimu mbalimbali zenye usarufi. Mofimu hizi ni za: ngeli, idadi, upatanishi wa kisarufi, mzizi na kadhalika. Aidha, kivumishi cha Kiimenti hudhihirisha mabadiliko mbalimbali ya sauti kinapoundwa. Makala haya yatasaidia kuendeleza usomi kuhusu vivumishi hasa katika lugha anuwai za kiasili. Kwa kuzingatia miundo ya kivumishi cha Kiimenti inayoibuliwa, tafiti zaidi zinaweza kufanywa katika lugha mbalimbali za Kiafrika ili kuweka wazi miundo ya vivumishi katika lugha husika.
2022-04-12T00:00:00+00:00Copyright (c) 2022 Chama Cha Kiswahili Afrika Masharikihttps://journals.chaka-ma.com/index.php/chakama/article/view/12UDUNISHAJI WA KIJINSIA KATIKA LUGHA YA KISWAHILI NA ATHARI YAKE KATIKA MAENDELEO YA JAMII2023-03-26T12:44:51+00:00Caroline Asiimwecaroline@chaka-ma.com
Dhana ya udunishaji wa kijinsia inahusu hali ya kuwakweza na kuwatweza mwanamume au mwanamke. Hali hii inatokana na jinsi lugha inavyowasilisha itikadi ya jinsia na namna inavyochangia kukweza na kutweza mwanamke na mwanamume katika jamii. Makala hii inafafanua namna lugha ya Kiswahili inavyoendeleza udunishaji wa kijinsia kwa kumtweza mwanamke huku mwanamume akikwezwa kutokana na itikadi ya kijamii na kijinsia pamoja na kuelezea athari yake katika maendeleo ya jamii. Kwa kuwa Kiswahili ni lugha ya mawasiliano mapana, makala hii inahoji kwamba matumizi yake katika kuzuia udunishaji wa kijinsia ni ya mustakabali mzuri. Ili kupata maendeleo katika jamii, makala hii inapendekeza lugha ya Kiswahili iangaliwe kama rasilimali muhimu katika maendeleo na kuitumia kama zana ya kijamii ambayo ni tendaji. Hali hii itaimarisha mawasiliano bora yanayozingatia upya namna itikadi za kijamii zinavyowasilishwa kwa kutumia lugha yenye ubunifu na uvumbuzi ili kuakisi masuala ambayo yanalenga maendeleo.
2022-04-12T00:00:00+00:00Copyright (c) 2022 Chama Cha Kiswahili Afrika Masharikihttps://journals.chaka-ma.com/index.php/chakama/article/view/13UKATAJI TAMAA MIONGONI MWA WATOTO KATIKA JAMII YA KISASA: TATHMINI KUTOKA RIWAYA YA KISWAHILI2023-03-26T12:48:39+00:00Naomi Nzilani MusembiMusembi@chaka-ma.com
Msukumo wa kuandika makala haya umetokana na ogezeko la haraka la visa mbalimbali vya watoto kujitoa uhai kutokana na ukataji tamaa vinavyoripotiwa katika vyombo vya habari. Hivi karibuni nchini Kenya, watoto wamekumbwa na tatizo la ukataji tamaa linalowapelekea wengi wao kujitoa uhai na kutoroka nyumbani. Wengi wao wanaishia kuishi mitaani kama ‘chokoraa’. Vilevile, ongezeko hili la ukataji tamaa linaonyesha ongezeko la viwango vya ushari katika jamii. Hili ni suala nyeti ambalo halipaswi kunyamaziwa. Linahitaji kushughulikiwa ili suluhu iweze kupatikana. Riwaya zilizohakikiwa ili kupata data toshelevu kuhusiana na mada hii ni Siku Njema ya Ken Walibora, Tumaini ya C. Momanyi na Yatima ya K. Wamitila. Utafiti unaoangazia changamoto wanazopitia watoto unahitajika ili kuwalinda kutokana na ukataji tamaa. Makala haya yanapania kuchunguza mambo ambayo yanaweza kutokea katika maisha ya mtoto ambayo yanaweza kuwa chanzo cha ukata tamaa. Vilevile, yatafafanua dalili za ukataji tamaa miongoni mwa watoto pamoja na kupendekeza suluhu za ukataji tamaa. Aidha, Makala haya yananuia kuchangia katika juhudi za kuelimisha umma kuhusu namna ya kupiga vita na kuangamiza vitendo vya ushari miongoni mwa wanajamii ambavyo huzua ukataji tamaa kwa watoto.
2022-04-12T00:00:00+00:00Copyright (c) 2022 Chama Cha Kiswahili Afrika Masharikihttps://journals.chaka-ma.com/index.php/chakama/article/view/14MATAPO YA UJAALA KATIKA JAMII ZA WATANZANIA2023-03-26T12:50:35+00:00Athumani S. Poneraponera@chaka-ma.comHassan R. Hassanhassan@chaka-ma.com
Makala hii inahusu ujaala. Dhana ya ujaala tunaitumia humu kumaanisha nguvu au kani inayotawala matukio yote yanayowatokea viumbe pasi na wao kuwa na uwezo wa kuzuia, kubadili, wala kudhibiti. Hoja kuu ya makala ni kutanabaisha kwamba mwanadamu razini huitambua, kuikiri na kuitumia kani hii katika kuviendesha vipengele mbalimbali vya maisha yake. Makala hii yenye mwegamo wa utamaduni inatokana na uchunguzi mpana wa utamaduni wa Watanzania. Data zilipatikana kupitia usomaji wa nyaraka pamoja na usaili. Makala imeundwa na sehemu kuu nne: Utangulizi, chimbuko na maendeleo ya dhana ya ujaala, matapo ya ujaala, na hitimisho. Makala inafafanua matapo makuu mawili ya ujaala ambayo jamii za Watanzania huyatumia pamoja na vijenzi vyake. Tapo la kwanza lililofafanuliwa ni ujaala wa kijadi. Vijenzi vya tapo hili ni makaburi, hirizi, milima, miti mikubwa, mapango pamoja na mkusanyiko wa maji mengi. Tapo la pili ni ujaala wa kisasa. Hili limegawanyika katika vijitapo vya ujaala wa Kikristo (vijenzi vyake ni Nabii Yesu Kristo, taasisi ya kanisa, na Biblia), ujaala wa Kiislamu (vijenzi vyake ni Mtume Muhammad, hadithi, msikiti, na Kur’an) pamoja na Ujaala wa
Kihindu (vijenzi vyake ni wanyama kama vile ng’ombe.
2022-04-12T00:00:00+00:00Copyright (c) 2022 Chama Cha Kiswahili Afrika Masharikihttps://journals.chaka-ma.com/index.php/chakama/article/view/15NAFASI YA JUMUIA YA AFRIKA MASHARIKI KATIKA KUENDELEZA KISWAHILI KAMA LUGHA YA KIMATAIFA2023-03-26T12:55:20+00:00Miriam OsoreOsore@chaka-ma.com
Jumuia ya Afrika Mashariki iliundwa 1967 na 1977. Mnamo mwaka 1999 ilianzishwa upya kupitia mkataba uliotiwa sahihi na mataifa anzilishi; Kenya, Uganda na Tanzania. Baadaye, mataifa ya Rwanda na Burundi yalijiunga mwaka wa 2007, huku Sudan ya kusini ikijiunga mwaka wa 2016. Lengo kuu la muungano huu lilikuwa kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa na kijamii kati ya mataifa wanachama. Maono ya jumuia ni kwamba hatimaye, nchi wanachama zitashirikiana katika maswala ya forodha na ushuru, kuwa na soko la pamoja, sarafu moja na mwishowe kuunda muungano wa kisiasa wa mataifa ya Afrika Mashariki. Jumuia hii ina asasi zinazoendeleza majukumu yake. Kati ya asasi hizi ni Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki. Katika kikao cha 35 cha baraza la mawaziri wa jumuia ya Afrika Mashariki kilichofanyika tarehe 4 Aprili 2017, Arusha, kati ya mambo yaliyojadiliwa ni azimio la bunge la
jumuia ya Afrika Mashariki (EALA) kuhusu kuteua Kiswahili kama mojawapo ya lugha rasmi za jumuia. Baraza hili lilijadili kuhusu urekebishaji wa sheria ya 137 ya mkataba ulioanzisha jumuia na kuelekeza nchi wanachama kuunda sera za kitaifa za Kiswahili ili kuimarisha matumizi yake katika nyanja zote rasmi. Vile vile mataifa wanachama yanahitajika kuanzisha michakato ya kuweka sheria za kufanya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya muungano kwa kuunda mabaraza ya kitaifa ya Kiswahili pamoja na vyama vya kitaifa vya Kiswahili. Kupitia jitihada hizi, Kiswahili kitapata nafasi katika orodha ya lugha kuu za kilimwengu. Ni katika muktadha huu ambapo
makala haya yanachunguza nafasi ya jumuia ya Afrika Mashariki katika kuendeleza Kiswahili kufika ulingo wa juu wa kimataifa. Makala pia imechunguza Yatachunguza hatua zinazoweza kuzingatiwa ili kuwezesha Kiswahili kuvuka mipaka hata zaidi na kuheshimiwa kama lingua franca ya bara la Afrika.
2022-04-12T00:00:00+00:00Copyright (c) 2022 Chama Cha Kiswahili Afrika Masharikihttps://journals.chaka-ma.com/index.php/chakama/article/view/16CHANGAMOTO ZA TAFSIRI TENGE KATIKA UFUNDISHAJI WA KISWAHILI KATIKA SHULE ZA SEKONDARI JIJINI KAMPALA2023-03-26T12:58:51+00:00George Mrikariamrikaria@chaka-ma.comSarah Ndanu M. Ngesusarah@chaka-ma.com
Makala haya yameonyesha kwamba matumizi ya tafsiri hususan uteuzi wa mikakati ya tafsiri katika ufundishaji wa lugha kama nyenzo ya kurahisisha mawasiliano hukabiliwa na changamoto mbalimbali. Data zilikusanywa kupitia ushuhudiaji na uchambuzi wa nyaraka. Kulingana na Cook (2018) tafsiri ni mchakato unaohusisha uteuzi wa mikakati ya tafsiri ambayo ndiyo msingi anaotumia mfasiri anapokabiliwa na tatizo la ukosefu wa visawe vya moja kwa moja baina ya lugha chanzi (kuanzia sasa LC) na lugha lengwa (kuanzia sasa, LL). Tafiti tangulizi Mohamed (2014), Ngwendu (2016), Ito (2017), Mahi (2018), Navidinia na wenzie (2019), Karimah (2020) na Ngesu (2020) kuhusu tafsiri na ufundishaji wa lugha ya kigeni hazijachunguza changamoto za uteuzi wa mikakati ya tafsiri katika hali halisi darasani ila zimejiegemeza kuchunguza changamoto za tafsiri kwa jumla. Uteuzi wa mikakati ya tafsiri isiyofaa unaweza kukwamisha mawasiliano katika ufundishaji na unaweza kuwa na athari hasi kwa mwanafunzi anayejifunza lugha. Hivyo, ilionekana ni muhimu kuchunguza uteuzi wa mikakati ya tafsiri katika mchakato halisi wa ufundishaji wa Kiswahili darasani. Matokeo yanaonesha kwamba walimu na wanafunzi hukabiliana na changamoto mbalimbali kutokana na kutumia mkakati wa tafsiri sisisi kwa lengo la kurahisisha mawasiliano. Inapendekezwa kuwa walimu ambao hawana maarifa na umahiri katika taaluma ya tafsiri waepuke kutumia tafsiri katika ufundishaji wa Kiswahili. Pia, inapendekezwa kuandaa warsha za mara kwa mara ili kuwasaidia walimu ambao tayari wamesoma kozi mbalimbali za tafsiri ili kuboresha umahiri wao katika tafsiri. Pia, inapendekezwa kuwawezesha walimu na wanafunzi kuwa na vitendeakazi kama vile kamusi thaniya na kamusi wahidiya.
2022-04-12T00:00:00+00:00Copyright (c) 2022 Chama Cha Kiswahili Afrika Mashariki