KISWAHILI NA LUGHA NYINGINE ZA KIAFRIKA KATIKA MAENDELEO YA AFRIKA MASHARIKI
Abstract
Makala hii inajaribu kutathmini namna ambavyo matumizi ya Kiswahili na lugha nyingine za KiAfrika yanaweza kuchangia maendeleo chanya na hasi. Dhana ya maendeleo imefafanuliwa ili kujumuisha sio tu ukuaji kiuchumi bali pia ukuaji wa demokrasia inayoruhusu ushiriki wa wananchi wote katika maamuzi juu ya masuala ya jamii wanamoishi. Mjadala umejikita katika maeneo matatu makuu ya maendeleo: uongozi na siasa; elimu na sekta ya uchumi isiyo rasmi. Kwa kutoa mifano ya matukio katika jamii pamoja na ithibati ya miradi ya utafiti iliyowahi kuendeshwa, imedhihirishwa kwamba Kiswahili na lugha nyingine za KiAfrika ni nguzo murua ambazo haziwezi kupuuzwa katika maendeleo ya Afrika Mashariki. Imeonyeshwa kwamba ijapokuwa kuna maendeleo hasi pamoja na changamoto wakati lugha hizi zinapotumika, upungufu uliobainishwa hautoshi kuzitupilia mbali lugha hizi. Hii ni kwa sababu kuna suluhu kwa changamoto hizo na kadri lugha yoyote inavyozidi kutumika ndivyo inazidi kuimarika ili kutekeleza majukumu ya maendeleo ya jamii.