MUUNDO WA VIVUMISHI VYA LUGHA ZA MNYAMBULIKO: MFANO WA KIVUMISHI CHA KIIMENTI
Keywords:
kivumishi, muundo, mofu, mofimu, mnyambuliko, lahajaAbstract
Kivumishi ni aina mojawapo ya maneno ambayo hutumika katika lugha sambamba na nomino ili kufanikisha mawasiliano. Ingawa tafiti nyingi zimefanywa kuhusu vivumishi, hatukuona utafiti wowote uliolenga miundo ya vivumishi katika Kiimenti. Makala haya yananuia kubainisha muundo wa kivumishi cha lahaja ya Kiimenti. Kiimenti ni mojawapo ya lahaja za Kimeru. Kimeru ni mojawapo ya lugha za Kibantu ambazo huzungumzwa nchini Kenya. Nia ya makala haya ni kuchunguza muundo wa kivumishi cha Kiimenti kwa kuongozwa na Nadharia ya Sarufi Geuza Maumbo Zalishi ambayo iliasisiwa na mwanaisimu Noam Chomsky (1957, 1965). Kupitia kwa nadharia hii, muundo wa nje na wa ndani wa kivumishi cha Kiimenti umewekwa wazi. Data ya utafiti huu ilipatikana kutokana na utafiti wa maktabani na nyanjani. Maktabani watafiti walisoma kazi mbalimbali zilizoangazia vivumishi vya Kiimenti. Utafiti wa nyanjani ulifanyika katika tarafa ya Abothuguchi Magharibi kwenye Kaunti ya Meru ambapo watafiti waliteua kimaksudi miktadha ya mikutano ya masoko na makanisa ili kukusanya data. Makala haya yanathibitisha kuwa kivumishi cha Kiimenti kinawasilisha muundo mahsusi na kikichanganuliwa kimofemiki kinaweza kuainisha mofimu mbalimbali zenye usarufi. Mofimu hizi ni za: ngeli, idadi, upatanishi wa kisarufi, mzizi na kadhalika. Aidha, kivumishi cha Kiimenti hudhihirisha mabadiliko mbalimbali ya sauti kinapoundwa. Makala haya yatasaidia kuendeleza usomi kuhusu vivumishi hasa katika lugha anuwai za kiasili. Kwa kuzingatia miundo ya kivumishi cha Kiimenti inayoibuliwa, tafiti zaidi zinaweza kufanywa katika lugha mbalimbali za Kiafrika ili kuweka wazi miundo ya vivumishi katika lugha husika.