UKATAJI TAMAA MIONGONI MWA WATOTO KATIKA JAMII YA KISASA: TATHMINI KUTOKA RIWAYA YA KISWAHILI
Abstract
Msukumo wa kuandika makala haya umetokana na ogezeko la haraka la visa mbalimbali vya watoto kujitoa uhai kutokana na ukataji tamaa vinavyoripotiwa katika vyombo vya habari. Hivi karibuni nchini Kenya, watoto wamekumbwa na tatizo la ukataji tamaa linalowapelekea wengi wao kujitoa uhai na kutoroka nyumbani. Wengi wao wanaishia kuishi mitaani kama ‘chokoraa’. Vilevile, ongezeko hili la ukataji tamaa linaonyesha ongezeko la viwango vya ushari katika jamii. Hili ni suala nyeti ambalo halipaswi kunyamaziwa. Linahitaji kushughulikiwa ili suluhu iweze kupatikana. Riwaya zilizohakikiwa ili kupata data toshelevu kuhusiana na mada hii ni Siku Njema ya Ken Walibora, Tumaini ya C. Momanyi na Yatima ya K. Wamitila. Utafiti unaoangazia changamoto wanazopitia watoto unahitajika ili kuwalinda kutokana na ukataji tamaa. Makala haya yanapania kuchunguza mambo ambayo yanaweza kutokea katika maisha ya mtoto ambayo yanaweza kuwa chanzo cha ukata tamaa. Vilevile, yatafafanua dalili za ukataji tamaa miongoni mwa watoto pamoja na kupendekeza suluhu za ukataji tamaa. Aidha, Makala haya yananuia kuchangia katika juhudi za kuelimisha umma kuhusu namna ya kupiga vita na kuangamiza vitendo vya ushari miongoni mwa wanajamii ambavyo huzua ukataji tamaa kwa watoto.