NAFASI YA JUMUIA YA AFRIKA MASHARIKI KATIKA KUENDELEZA KISWAHILI KAMA LUGHA YA KIMATAIFA
Keywords:
lugha ya Kimataifa, Lugha Rasmi, Lingua FrancaAbstract
Jumuia ya Afrika Mashariki iliundwa 1967 na 1977. Mnamo mwaka 1999 ilianzishwa upya kupitia mkataba uliotiwa sahihi na mataifa anzilishi; Kenya, Uganda na Tanzania. Baadaye, mataifa ya Rwanda na Burundi yalijiunga mwaka wa 2007, huku Sudan ya kusini ikijiunga mwaka wa 2016. Lengo kuu la muungano huu lilikuwa kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa na kijamii kati ya mataifa wanachama. Maono ya jumuia ni kwamba hatimaye, nchi wanachama zitashirikiana katika maswala ya forodha na ushuru, kuwa na soko la pamoja, sarafu moja na mwishowe kuunda muungano wa kisiasa wa mataifa ya Afrika Mashariki. Jumuia hii ina asasi zinazoendeleza majukumu yake. Kati ya asasi hizi ni Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki. Katika kikao cha 35 cha baraza la mawaziri wa jumuia ya Afrika Mashariki kilichofanyika tarehe 4 Aprili 2017, Arusha, kati ya mambo yaliyojadiliwa ni azimio la bunge la
jumuia ya Afrika Mashariki (EALA) kuhusu kuteua Kiswahili kama mojawapo ya lugha rasmi za jumuia. Baraza hili lilijadili kuhusu urekebishaji wa sheria ya 137 ya mkataba ulioanzisha jumuia na kuelekeza nchi wanachama kuunda sera za kitaifa za Kiswahili ili kuimarisha matumizi yake katika nyanja zote rasmi. Vile vile mataifa wanachama yanahitajika kuanzisha michakato ya kuweka sheria za kufanya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya muungano kwa kuunda mabaraza ya kitaifa ya Kiswahili pamoja na vyama vya kitaifa vya Kiswahili. Kupitia jitihada hizi, Kiswahili kitapata nafasi katika orodha ya lugha kuu za kilimwengu. Ni katika muktadha huu ambapo
makala haya yanachunguza nafasi ya jumuia ya Afrika Mashariki katika kuendeleza Kiswahili kufika ulingo wa juu wa kimataifa. Makala pia imechunguza Yatachunguza hatua zinazoweza kuzingatiwa ili kuwezesha Kiswahili kuvuka mipaka hata zaidi na kuheshimiwa kama lingua franca ya bara la Afrika.