CHANGAMOTO ZA TAFSIRI TENGE KATIKA UFUNDISHAJI WA KISWAHILI KATIKA SHULE ZA SEKONDARI JIJINI KAMPALA
Keywords:
Tafsiri, Tafsiri Sisisi, UfundishajiAbstract
Makala haya yameonyesha kwamba matumizi ya tafsiri hususan uteuzi wa mikakati ya tafsiri katika ufundishaji wa lugha kama nyenzo ya kurahisisha mawasiliano hukabiliwa na changamoto mbalimbali. Data zilikusanywa kupitia ushuhudiaji na uchambuzi wa nyaraka. Kulingana na Cook (2018) tafsiri ni mchakato unaohusisha uteuzi wa mikakati ya tafsiri ambayo ndiyo msingi anaotumia mfasiri anapokabiliwa na tatizo la ukosefu wa visawe vya moja kwa moja baina ya lugha chanzi (kuanzia sasa LC) na lugha lengwa (kuanzia sasa, LL). Tafiti tangulizi Mohamed (2014), Ngwendu (2016), Ito (2017), Mahi (2018), Navidinia na wenzie (2019), Karimah (2020) na Ngesu (2020) kuhusu tafsiri na ufundishaji wa lugha ya kigeni hazijachunguza changamoto za uteuzi wa mikakati ya tafsiri katika hali halisi darasani ila zimejiegemeza kuchunguza changamoto za tafsiri kwa jumla. Uteuzi wa mikakati ya tafsiri isiyofaa unaweza kukwamisha mawasiliano katika ufundishaji na unaweza kuwa na athari hasi kwa mwanafunzi anayejifunza lugha. Hivyo, ilionekana ni muhimu kuchunguza uteuzi wa mikakati ya tafsiri katika mchakato halisi wa ufundishaji wa Kiswahili darasani. Matokeo yanaonesha kwamba walimu na wanafunzi hukabiliana na changamoto mbalimbali kutokana na kutumia mkakati wa tafsiri sisisi kwa lengo la kurahisisha mawasiliano. Inapendekezwa kuwa walimu ambao hawana maarifa na umahiri katika taaluma ya tafsiri waepuke kutumia tafsiri katika ufundishaji wa Kiswahili. Pia, inapendekezwa kuandaa warsha za mara kwa mara ili kuwasaidia walimu ambao tayari wamesoma kozi mbalimbali za tafsiri ili kuboresha umahiri wao katika tafsiri. Pia, inapendekezwa kuwawezesha walimu na wanafunzi kuwa na vitendeakazi kama vile kamusi thaniya na kamusi wahidiya.