TATHMINI YA SERA ZA LUGHA KATIKA SEKTA YA ELIMU NCHINI KENYA: HALI YA SASA YA KISWAHILI KATIKA MTAALA MPYA
Abstract
Sera ya lugha katika sekta ya elimu katika nchi yoyote ile ni muhimu kwa vile ndiyo huamua jukumu la kila lugha katika elimu. Nchini Kenya sera hizi zimepitia mabadiliko mengi yanayoweza kuangaliwa miaka ya nyuma yanayoanza wakati wa ukoloni hadi sasa. Sera hizo zinahusisha Kiingereza, Kiswahili na lugha zingine asilia. Sera hizi zimeeleza namna kila lugha inafaa kutumika katika kufanikisha shughuli za kufundisha na kujifunza katika kila kiwango. Ingawa lugha ya Kiswahili inatambulika kama lugha rasmi na ya taifa nchini Kenya, katika mtaala mpya wa elimu haijapewa nafasi muhimu inavyostahili. Hali hii huenda imetokana na sera za lugha za awali kuanzia wakati wa ukoloni hadi sasa. Makala hii inatathmini sera za lugha katika sekta ya elimu nchini Kenya kuanzia wakati wa ukoloni hadi sasa ili kuonesha namna sera hizo zimachangia hali ya sasa ya Kiswahili katika mtaala mpya. Kadhalika, makala hii inaangazia nafasi ya Kiswahili katika mtaala mpya huku ikitoa mapendekezo.