UTAFITI WA ISIMU YA KISWAHILI KATIKA VYUO VIKUU
Abstract
Utafiti wa isimu ya Kiswahili ni nguzo muhimu ya ufundishaji na maendeleo ya Kiswahili. Ili lugha ipate kukua na kuendelea, kuna haja ya kufanya utafiti zaidi katika sarufi ya lugha husika. Kwa muda mrefu, isimu ya Kiswahili imefanyiwa utafiti na kufunzwa katika vyuo vikuu. Hata hivyo, utafiti wa isimu ya Kiswahili katika vyuo vikuu umezongwa na changamoto/matatizo si haba. Changamoto hizi zinahusu idadi ya tafiti, nadharia za isimu na umakinifu unaoendana na utafiti wa isimu ya Kiswahili vyuoni. Hali hii imechangia ufundishaji wa isimu ya Kiswahili kukumbwa na uhaba wa walimu na vitabu/marejeleo, kutofundishwa kwa nadharia za isimu na tafiti chache katika mawanda yote ya isimu ya Kiswahili. Kutokana na changamoto hizi, idadi ya wanafunzi wa isimu ya Kiswahili ni ndogo mno. Makala haya yanalenga kutathmini na kujadili changamoto zilizoko katika utafiti wa isimu ya Kiswahili vyuoni. Hususan, silabi za Kiswahili zimepewa nafasi ndogo katika utafiti na ufundishaji vyuoni. Hii ndio sababu kumekuwa na mielekeo tofautitofauti kuhusu silabi za Kiswahili. Utafiti umeonyesha kwamba silabi ina jukumu muhimu katika sarufi ya lugha yoyote ile, ikiwemo Kiswahili. Makala haya vilevile yananuia kuonyesha umuhimu wa kutafiti na kufunza silabi za Kiswahili kwa kutumia nadharia mahsusi za kiisimu. Mbali na kutathmini changamoto hizi, makala haya yanalenga kutoa mapendekezo ya kuimarisha utafiti na ufunzaji wa isimu ya Kiswahili vyuoni.